KINOLE SACOS KARIBU YAKO

+255 784 228 854

Tufuatilie :
WhatsApp-Image-2025-02-11-at-13.44.03_30307140-e1745589993949
Kinole Saccos 

Mikopo kwa Wanachama
Home » Mikopo kwa Wanachama

Kinole Saccos inatoa Mikopo ya aina kumi

Mikopo ya Biashara

Huu ni mkopo utakaotolewa kwa ajili ya kuendeleza biashara kama vile maduka ya jumla na rejareja, kuuza na kuhifadhi nafaka na biashara nyingine zote halali. Mkopo huu utatolewa kwa mwanachama ambaye tayari anafanyabiashara.

Mkopo huu utakuwa unarejeshwa kwa kila mwezi au mwishoni mwa makatab kwa biashara za kuhifadhi mazao, kwa muda usiozidi miaka 3. Mkopo utakaolipwa mwishoni utakuwa na riba 2.5% kwa mwezi lakini utakaolipwa kila mwezi riba yake itakuwa asilimia 17 kwa mwaka.

Mkopo utakuwa na bima kama inavyooneshwa katika jedwali namba 01 lililoambatanishwa na sera hii. Mkopo utakuwa na ada ya uchakataji wa 0.5% ya mkopo utakaoidhinishwa. Mkopo huu utaanzia TZS 50,000 lakini hautazidi TZS 100,000,000.

Mikopo ya Ujenzi

Huu ni mkopo kwa ajili ya kuwawezesha wanachama kujijengea nyumba bora za kuishi ama biashara. Mkopo utajumuisha ununuzi wa kiwanja, ujenzi wa jengo, maboresho na ukarabati wa jengo. Mkopo huu unaweza kulipwa kila mwezi au mwishoni mwa muda wa mkopo kutegemea na shughuli za mkopaji.

Mkopo huu utaanza kulipwa kwa makubaliano na mkopaji juu ya utaratibu wa marejesho, muda wa mkopo hautazidi miaka 3. Riba ya mkopo itakiuwa 15% kwa mwaka endapo utalipwa kila mwezi na 2% endapo utalipwa mwisho, na utalipiwa bima kama ilivyoonyeshwa katika jedwali namba 01. Mkopo pia utakuwa na ada ya uchakataji wa 0.5% ya mkopo utakaoidhinishwa. Mkopo huu utaanzia TZ 50,000 lakini hautazidi TZS 40,000,000.

Mikopo ya Kilimo

Huu ni mkopo kwa ajili ya shughuli za kilimo na ufugaji na utazingatia kalenda ya zao/mifugo husika au shughuli iliyopo shambani na utalipwa mwishoni mwa msimu kwa mkupuo mmoja au kila mwezi kutegemea na aina ya zao au shughuli itakayofanyika shambani.

Mkopo utakaolipwa mwishoni utakuwa na riba 2.0% kwa mwezi lakini utakaolipwa kila mwezi riba yake itakuwa 15% kwa mwaka. Mikopo yote hii itakuwa na bima kama ilivyoonyeshwa katika jedwali namba 01. Mkopo pia utakuwa na ada ya uchakataji wa 0.5% ya mkopo utakaoidhinishwa. Mkopo  huu utaanzia TZS 50,000 lakini hautazidi TZS 30,000,000.

Mikopo ya Dharura

Huu ni mkopo kwaajili ya kukabiri matukio ya dharula ikiwemo misiba, kuuguza, kuunguliwa moto, mafuriko, matetemeko na matukio mengine kama hayo. Mkopo utakuwa wa muda usiozidi miezi 6. Kwa mkopo utakaolipwa kila mwezi, riba itakuwa 1.25% kwa mwezi wakati mkopo utakaolipwa mwishoni, riba yake itakuwa asilimia 2% kwa mwezi. Mikopo hii itakuwa na bima kama ilivyoonyeshwa katika jedwali namba. kiwango cha mkopo wa dharula kitaanzia TZS 50,000 lakini hakitazidi TZS 500,000.

Mikopo ya Vyombo vya Moto

Huu utakuwa ni mkopo kwa ajili ya ununuzi au ukarabati mkubwa wa magari, bajaji na pikipiki. Huu utakuwa ni mkopo utakaotolewa kwa muda usiozidi miaka miwili na muda wa rehema wa kuanza marejesho kwa miezi 3. Muda wa mkopo kwa mkopo wa ununuzi wa magari utakuwa hadi miezi 24,  kwa ununuzi wa Bajaji utakuwa hadi miezi 18 na kwa pikipiki utakuwa hadi miezi 15.

Mikopo ya ukarabati wa vyombo vya moto hautazidi mwaka mmoja. Mkopo utakuwa na riba ya 2.5% kwa mwezi wakati wa muda wa rehema, na muda uliobaki utatozwa 17% kwa mwaka.

Mkopaji atatakiwa kulipia bima ya mkopo kama ilivyo katika jedwali namba 01 na mkopaji atatakiwa kulipia gharama za maandalizi ya mkopo ya 0.5%. Aidha kadi ya chombo kilichonunuliwa kwa mkopo huu itahifadhiwa na SACCOS hadi mwanachama atakapomaliza marejesho ya mkopo.

Aidha chombo husika kitatakiwa kukatiwa bima kubwa kwa kipindi chote cha mkopo. Kiasi cha mkopo kitaanzia TZS 50,000 lakini hakitazidi TZS 100,000,000.

Mikopo ya Elimu

Huu ni mkopo kwa ajili ya kusomesha ama kujiendeleza kielimu kwa ngazi zote za elimu na utatolewa kwa kiasi kinacholingana na malipo yanayotakiwa kulipwa katika taasisi husika na gharama za ziada zitakazohitajika. Hata hivyo  mkopo huu hautazidi TZS 5,000,000 (milioni tano tu).

Mkopo utakuwa na riba ya 10% kwa mwaka kwa muda usiozidi mwaka mmoja na unaweza kulipwa kila mwezi au kila robo mwaka. Mkopaji atatakiwa kulipia bima ya mkopo kama ilivyo katika jedwali namba 01 na mkopaji atatakiwa pia kulipia gharama za maandalizi ya mkopo ya 0.5%.

Mikopo ya Kikundi

Mkopo huu utawahusu wajasiriamali wadogo ambao kabla ya kupatiwa mkopo watakuwa wamejiunga kama kikundi kinachotambuliwa na serikali ya kijiji walipo kwa idadi isiyopungua watu watano. Kikundi kitatakiwa kuomba uanachama kama wanachama wengine. Mkopo utatolewa baada ya kupatiwa mafunzo maalum ya mikopo kwa kikundi husika,

mkopo utategemea kiasi cha akiba za kikundi na mkopo utatolewa katika ngazi tatu – ngazi ya awali mkopo utakuwa hadi mara mbili ya akiba kwa miezi sita, ngazi ya pili mkopo utakuwa hadi mara tatu ya akiba za kikundi kwa muda wa mwaka mmoja na ngazi ya tatu mkopo hautazidi mara tano ya akiba za kikundi kwa muda usiozidi miaka miwili.

Mkopo utakuwa na riba ya asilimia 20 kwa mwaka na utakuwa na bima ya mkopo kama ilivyo katika jedwali namba 01 na mkopaji atatakiwa kulipia gharama za maandalizi ya mkopo ya 0.5%. Kikundi kitakachofikia hatua ya tatu wanachama wake watashauriwa kujiunga na SACCOS mmoja mmoja na kuomba mikopo binafsi.

Mikopo ya Vifaa vya 
Matumizi Mbalimbali 

Mkopo huu ni kwaajili ya mahitaji ya samani na vyombo kwa wanachama. Mkopo huu utatolewa kwa mkopaji kupatiwa vifaa visivyozidi thamani ya TZS 2,000,000. Kinole SACCOS itashikilia hati ya kifaa husika mpaka mkopaji atakapomaliza kulipa mkopo wake.

Kwa mkopaji ambae tayari ana mkopo mwingine, anatakiwa awe amelipa mkopo wake  kwa angalau  50% ndipo aweze kupatiwa mkopo huu.

Muda wa mkopo huu hautazidi miezi kumi na mbili tu. Riba ya mkopo huu itakuwa ni 15% kwa mwaka.  Mkopo utakuwa na ada ya mkopo ya 0.5% ya mkopo utakaoidhinishwa pamoja na bima ya mkopo kama ilivyo katika jedwali namba 01.

Mikopo ya Ununuzi wa mali zisizohamishika. 

Huu ni mkopo kwa ajili ya ununuzi wa mali zisizohamishika kama vile mashamba, viwanja na nyumba. Katika aina hii ya mkopo mali inayonunuliwa ndiyo dhamana ya mkopo husika.

Kinole SACCOS itasimamia zoezi la mauziano ya mali husika na hati ya mauziano itahifadhiwa na Kinole SACCOS hadi marejesho ya mkopo yatakapomalizika.

Kima cha chini kitakuwa ni TZS 50,000 lakini mkopo hautazidi TZS 30,000,000 kwa muda usiozidi miaka mitatu kwa riba ya 15% kwa mwaka kwa mkopo wa kulipa kila mwezi na 2% kila mwezi kwa mkopo utakaolipwa mwisho, na utalipiwa bima kama ilivyo katika jedwali namba 01 na mkopaji atatakiwa kulipia gharama za maandalizi ya mkopo ya asilimia 0.5 .

Mikopo ya Watumishi wa Chama

Mkopo Huu ni mkopo utakaotolewa kwa watendaji wa chama walioajiliwa kwa mikataba ya muda maalumu au mikataba ya kudumu ili kuwasaidia kupunguza ukali na ugumu wa maisha na waweze kujiendeleza katika nyanja mbalimbali. Marejesho ya mkopo huu yatakuwa yanakatwa mojakwamoja kutoka katika mshahara wa mtendaji kwa kila mwezi.

Kiasi cha mkopo huu ni kuanzia TZS 500,000 hadi TZS 30,000,000 na muda wa mkopo ni hadi miezi 36 lakini mkopo utatolewa kulingana na muda wa mkataba uliobaki wa mtendaji husika wakati anaomba mkopo.

Riba ya mkopo huu itakuwa 10% kwa mwaka, mkopaji atakatwa bima kama inavyoonekana katika Jedwali namba 01 na ada ya mkopo ya 0.5%, na mtumishi hatalazimika kuwa na akiba ya kuombea mkopo.